- Shemot / Kutoka 33:12-34:26
- Bamidbar / Hesabu 28:19-25
- Yekhezekiel / Ezekieli 36:37-37:14
- Korintim Alefu / 1 Wakorintho 5:6-8
Shemot {33:14} HaShem akajibu, “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa pumziko. {33:15} Kisha Moshe (Mose) akamwambia, “Kama uso wako hauendi pamoja nasi, usituondoe hapa. {33:16} Mtu ye yote atajuaje kuwa mimi pamoja na watu wako tumepata kibali mbele Zako, usipokwenda pamoja nasi? Ni nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu Wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
Moshe (Mose) alijua jinsi uwepo wa Mungu ulivyowapasa bnei Yisraeli (wana wa Israeli). Bila ya Uwepo wa Mungu wangalikuwa kama mataifa mengine duniani. Moshe alishapitia uzoefu wa kujua ilikuwaje kuishi kati ya mataifa mengine ambako hakukuwepo na uwepo wa Mungu. Moshe alikwisha ishi kote, Mitsirayim (Misri) na Midiani, hivyo alijua hasa ilikuwaje kuishi katika mataifa yanayoabudu sanamu. Sasa baada ya tukio la kichaka kiwakacho moto, juu mlimani, hakutaka kabisa kurudi bila ya kuwa na uwepo wa Mungu kuwa pamoja naye.
Si vigumu kwangu kudhania kwamba Moshe alikuwa amejitoa sana kwa HaShem na kushaukia kwa makini uhusiano wake Naye kiasi cha kwamba hakuwa tayari kwenda mahali popote bila ya uwepo wa Mungu. Je, unakumbuka sababu aliyoitoa ya uwepo wa Mungu kwenda pamoja na bnei Yisraeli? “… nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu Wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
Moshe alijua kwamba uwepo wa Mungu katika maisha ya mtu, ulimfanya kuwa tofauti. Hakika ulimfanya kuwa tofauti sana na taifa jingine lolote katika uso wa dunia.
Je, inamaanisha nini kuwa katika uwepo wa Mungu? Tunapokuwa katika uwepo wa Mungu, Yeye anakuwa ni dira yetu ya kudhatitiwa sana. Kuna nguvu katika uwepo wa Mungu, bnei Yisraeli hawakuhitaji kuogopa taifa lolote lile, ili mradi tu uwepo wa Mungu ulikuwa nao maana hakuna taifa lolote lingeweza kuwashinda. Hakuna hofu katika uwepo wa Mungu, ila kuna toba, kuna msamaha na kuna mabadiliko ya tabia. Na kusema kweli katika uwepo wa Mungu kuna kuongozwa, kuelekezwa, mafunuo ya kinabii, faraja na amani. Si ajabu kwamba Moshe hakutaka kuukosa uwepo wa Mungu. Je, wewe vipi?
Shabbati hii tunasherekea siku inayofuatia sikukuu ya Pasaka. Kwetu sisi Pasaka ni juu ya kifo na ufufuko wa Yeshua HaMashiakhi. Kila sehemu inayohusiana na sherehe ya Pasaka, kwa upande fulani ni kielelezo cha kile Mashiakhi alitufanyia sisi. Kwa nini Mashiakhi ilimbidi aje duniani na kufa? Alikuja na kufa ili tuweze kuokolewa, lakini pia ni kwa sababu hii:
Yokhanani (Yohana) {16:7} Lakini amin nawaambia, yafaa Mimi niondoke kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu.
Yokhanani {14:26} Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Ruakhi HaKodeshi (Roho Mtakatifu), ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina Langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. {14:27} Amani nawaachia, amani Yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
Bnei Yisraeli hawakuwa na nabii kabla ya Yeshua HaMashiakhi; yaani Mungu katika mwili ajaye duniani kama mwanadamu. Na kusema kweli hawakuwa na uwepo wa Mungu; maana uwepo Wake uliondoka katika Bet HaMikdashi (Hekalu) kama tulivyoelezewa na nabii Yekhezkeli (Ezekieli) katika ukurasa wa 10 na 11 wa kitabu chake. Mwishoe baada ya zaidi ya miaka mia nne, Mashiakhi alikuja na bnei Yisraeli tena walikuwa na uwepo wa Mungu. Walakini, Yeshua alikuwa karibu kuondoka, Alihitaji kuchukua nafasi Yake mbinguni ili kukamilisha sehemu ya muhimu kwa ajili yetu na harakati ya ukombozi wa ulimwengu, bali HaShem wakati huu hakutaka kutuacha bila ya uwepo Wake. Hivyo Alimpeleka Ruakhi HaKodeshi kuwa pamoja nasi.
Yokhanani {14:16} "Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele; {14:17} Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.
Kila mtu amwaminiye Yeshua HaMashiakhi ana uwepo wa Mungu ukiishi ndani yao, “… nini kingine kitakachoweza kututofautisha mimi na watu Wako miongoni mwa watu wengine wote walio katika uso wa dunia?”
Je, unaweza kusema hakika unaishi maisha ya kuwekwa kando?
Enjoyed this Post? Subscribe to our RSS Feed, Follow us on Twitter, make a Comment or simply recommend us to friends and colleagues!

Bookmark

Write to us








